POLISI YATAKIWA KUWEKA USAWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 Vyama vya siasa nchini vimeliomba Jeshi la Polisi kutenda haki na kutoonyesha kupendelea upande wowote kuelekea kwenye uchaguzi, ili kutunza amani na utulivu.

Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, kwa kazi nzuri ya kulinda raia na mali zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema iwapo jeshi hilo litasimamia sheria, kanuni na taratibu bila ubaguzi au kubeba chama chochote cha siasa, hakutakuwa na uvunjifu wa amani utakaotokea.

Viongozi hao walikuwa wakizungumzia kauli ya IGP Simon Sirro, aliyoitoa mwanzoni mwa wiki akihojiwa na Kituo cha luninga cha ITV, ambaye aliwaonya wanasiasa wanaoanzisha shari kupitia matamshi yao.

Msemaji wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tumaini Makene, alisema CHADEMA inashangazwa namna ambavyo Polisi hawajachukua hatua kwa watu waliotoa kauli za vitisho dhidi ya mgombea urais wao, Tundu Lissu, ambazo zinaashiria shari na kutaka kuvuruga amani.

“Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alishamwandikia barua IGP ili achukuliwe hatua dhidi ya waliotaka kumuua Lissu mwaka 2017 na wanaotoa lugha za kutishia uhai wake, hadi sasa hakuna majibu na badala yake kinachozungumzwa ni kitu kingine,” alisema.

Alisema chama hicho kitafanya siasa kwa mujibu wa kanuni na sheria za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na kwamba kampeni zao zote zitazingatia hayo na si maelekezo ya polisi.

“Kama polisi wanataka uchaguzi uwe wa amani na utulivu watende haki, waachie wananchi wafanye uamuzi kwenye sanduku la kura, kusiwe na maelekezo ya mara kwa mara kwa vyama,” alisema.

Makene alitolea mfano wa matukio ya hivi karibuni ya mgombea wa ubunge Jimbo la Ruangwa kusakwa na polisi, huku wanachama wao waliokuwa wanamsindikiza mgombea ubunge huko Mpwapwa kurejesha fomu kukamatwa.

“Jeshi la Polisi litende haki kwa vyama vyote, tunafahamu maadili na sheria na si kwa maelekezo ya jeshi la polisi,” alibainisha.


Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post

Disqus Shortname

sigma2

Contact Form