MAGONJWA YA AKILI HUWAATHIRI ZAIDI WANAUME

IDADI ya wagonjwa wa akili imeongezeka kutoka 29,166 mwaka 2018/19 hadi 33,287 mwaka 2019/20 huku wanaume wakiongoza, imeelezwa.


Haya yalisemwa jana ikiwa leo ni Siku ya Afya ya Akili Duniani na kwamba idadi hiyo ya wagonjwa ni wale kwa waliotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Upanga na Mloganzila, jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya wagonjwa hao idadi ya wanaume ni kubwa ambao walikuwa 18,535 kulinganisha na wanawake ambao walikuwa 10,631 kwa mwaka 2018/19.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili MNH, Dk Fileuka Ngakongwa, aliyabainisha hayo jana mbele ya waandishi wa habari wakati akizungumzia maadhimisho hayo.


Akizungumzia sababu za wanaume wengi kuugua matatizo ya akili na kupata ugonjwa huo katika umri mdogo, ukilinganisha na wanawake, alisema ni kutokana na msongo wa mawazo, ugumu wa maisha na kuweka vitu moyoni kulinganisha na wanawake ambao huzungumza.


“Uwiano wa ugonjwa huu wa akili kati ya wanaume na wanawake ni mbili kwa moja, wanaume ni wengi ukilinganisha na wanawake,” alisisitiza.


Alieleza sababu nyingine za ugonjwa huo ni uwezo binafsi wa kuchanganua changamoto anazopitia kwenye maisha na jamii inayomzunguka.


Alisema pia mazingira ya watu wanayoishi, wanayofanyia kazi, kukosa amani, vinasaba vya akili na magonjwa ya mwili kama Malaria, Homa ya Kichwa na Uti wa Mgongo, ajali ya kichwa na wenye maambuzi ya UKIMWI kwenda kichwani na magonjwa yasiyoambukiza.


“Niwasihi Watanzania kujitokeza kupata huduma za afya pindi wanapohisi kuwa na dalili za ugonjwa huu wa akili kwa sababu unatibika kwa muda mfupi endapo mgonjwa atawahi hospitali,” alisema Dk. Ngakongwa.


Alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kukosa usingizi, unywaji wa pombe kupita kiasi, woga uliopitiliza, mtoto kukojoa kitandani katika umri ambao alishapita hatua hiyo.


Alisema licha ya kutoa huduma hiyo kwa mafanikio makubwa kuna changamoto ya wagonjwa kutelekezwa hospitali na ndugu, jamaa na marafiki.


Dk. Ngakongwa alisema, ndugu wa wagonjwa wanapofika hospitali kuwaleta ndugu huwaacha solemba hivyo, hospitali hulazimika kuwatafuta ndugu zao mahali popote nchini na kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kwa sababu matibabu yake huusisha familia na watoa huduma.



Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post

Disqus Shortname

sigma2

Contact Form