BABA JELA KWA KUMBAKA BINTI YAKE

Mahakama ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, imemhukumu Makoye Mwinamila kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya mkazi huyo wa Kijiji cha Mulumba, Kata ya Bwina wilayani hapa, kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kambo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana baada ya Upande wa Mashtaka kukamilisha maelezo na ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama hiyo.

Makoye Mwinamila alifikishwa mahakamani hapo akidaiwa kufanya ukatili huo dhidi ya mtoto huyo (jina tunalihifadhi) baada ya kumwacha mkewe sokoni akiuza mahindi.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anosisye Erasto, akishirikiana na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mauzi Lyawatwa, walidai mahakamani kuwa mshtakiwa alitenda ukatili huo, akimtishia kumuua iwapo angepiga kelele wakati akimwingilia kingono.

Walidai mahakamani hapo kuwa kitendo cha kumwingilia mtu kimwili pasipo ridhaa yake ni kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) pamoja na cha 131(3) cha Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kabla ya mtoto huyo kutendwa ukatili huo, baba na mama waliondoka nyumbani kwao majira ya asubuhi na kwenda Kitongoji cha Budili kuuza mahindi.

Ilidaiwa kwamba, wakiwa Budili, hali ya hewa ilibadilika na kuonyesha mawingu mazito ya mvua hivyo mke wa mshtakiwa, Paulina John, akamshauri mumewe kurudi nyumbani ili kuondoa mahindi yaliyokuwa yameanikwa juani.

Ilidaiwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kuwa, mama aliwaona watoto wake wanne wadogo wakifika eneo lake la biashara huku binti yake (mwathirika wa tukio) akiwa kabaki nyumbani, na alipotaka kufahamu sababu za kwenda eneo lake la biashara, walimweleza kuwa baba yao ndiyo kawaagiza.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, kutokana na hali hiyo, mama wa watoto hao alilazimika kurejea nyumbani haraka na kumkuta mumewe kitandani akifanya ukatili huo dhidi ya mwanaye na akalazimika kupiga yowe kuomba msaada kwa majirani, waliojitokeza na kumkamata mshtakiwa.

Baada ya maelezo ya pande zote, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Odira Amworo, alisema mahakama yake imejiridhisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa anayo hatia, lakini akampa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu.

Mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa madai kuwa hilo ni kosa lake la kwanza kutenda kwa kipindi chote cha maisha yake na kwamba anategemewa na familia pamoja na wazazi wake ambao ni wazee.

Licha ya utetezi huo, mahakama ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela, Hakimu Amworo akisema adhabu hiyo inapaswa kuwa fundisho kwa watu wengine ambao wamekuwa wakifanya au kukusudia kufanya ngono pasipo ridhaa ya wenzao.
Previous Post Next Post

Disqus Shortname

sigma2

Contact Form